Saturday, May 15, 2010

Eureka!

Immaculate Virgin - Sanamu ya Bikira


San Cristobal Hill (Cerro San Cristobal)


Ni mara chache sana huwa ninafikiwa na kuitambua hali ambayo ilinifikia nilipokuwa juu ya kilima cha San Cristobal. Pengine hali hiyo haijawahi kukufikia – au haujawahi kuitambua katika maana hii - na kama bado basi lazima itakufikia.


Pamoja na shughuli za mkutano, maongezi, matembezi na kadhalika, bila ya kutarajia nilipokuwa nimeketi nikiuangalia mji mzima wa Santiago na vilele vya milima ya Andes (au moshi unaotokana uchafuzi wa hali ya hewa unaozuia kuonekana vilele vya milima hiyo) hali kama ya ufunuo wa namna fulani ilinivaa nikatota ndani ya hali hiyo ya uwepesi wa mawazo, mawazo yaliyokuwa wazi ambayo yalinifafanulia muelekeo wa maisha.


Kama vile taa iliwashwa katika giza. Kila kitu kiliwekwa wazi na busara ya hali juu ilifunuliwa. Kila kipande cha kitendawili kiliangukia kwenye nafasi yake. Nilijawa na matumaini makubwa. Majawabu yote yaliwekwa mbele yangu. Furaha ikanijaa. Nilipata nguvu – ningeweza kupambana na chochote, ningeweza kuelewana na yeyote ambaye kwa sababu moja au nyingine pengine hatuwezi kuafikiana na kuwa na heri kati yetu.


Sikutaka kusogea hata kwa inchi moja au kufanya lolote ili niendelee kuwa ndani ya hali ile daima. Basi, hali ile haikudumu, kadiri nilivyong’ang’ania kuishikilia ndivyo ilivyozidi kuniponyoka.


Haidhuru, hali ile ilifanya ilichotumwa. Kwamba nimeona, naomba nipate nguvu ya kufuatilia kwa makini mawazo yale mema.

0 comments: