Chema hakidumu kingekupendeza
Ungawa na hamu kukingojeleza
Saa ikitimu kitakuteleza
Chema wangu babu Kibwana Bashee
Alojipa tabu kwamba anilee
Illahi Wahabu mara amtwee
Hizo beti mbili nilizikariri zamani kutoka kwenye kitabu cha Abdilatif Abdala "Sauti ya Dhiki". Na kama ninavyozikumbuka zimekuwa zinanizinga mawazoni kwa masiku kadhaa sasa.
Nimeingiwa na machungu na woga. Uwezo wangu wa kufikiri au kutatua matatizo yaliyonifika umeniponyoka. Maisha yamenikumbusha uwanaadamu wangu. Kinachonisukuma ni ule moyo wa stahamali tu. Na ninaomba nijaaliwe stahamali zaidi.
Kitambo kidogo kilichopita Mwenyezi Mungu alimtwaa kipenzi Mama yangu Mkubwa, Kadala. Marehemu Kadala nilikuwa naye karibu sana wakati wa utoto wangu.
Naam, ndio maisha. Na hapa nilipo maisha mengine yanaenda kwa kasi ya mwendo wa radi. Nakimbiakimbia, ninachakurachakura kama kuku kutwa nzima. Kukicha naanza tena kama jana. Ndio maisha.
Basi naona bora kukawia kuliko kuiwacha safari. Tupo wote safarini japo tunaonana kwa nadra bloguni. Mambo yakisawazika bila ya shaka nitaongeza kasi na huku kwenye mitandao pia.
Haidhuru. Kule kwenye kurasa za Global Voices baada ya muda kama mwezi hivi kuna muhtasari wa blogu za kiswahili uliopandishwa leo. Tafadhali tupa jicho na huko pia. Bila kusahau kuperuzi kidogo kwenye ukurasa wa Reuters Tanzania.
Monday, May 07, 2007
Subscribe to:
Posts (Atom)