Hatimaye serikali ya Australia imeitikia wito uliotolewa mwezi wa nne mwaka huu na gazeti la
Zimdaily,
wa kuwafukuza watoto wa viongozi wa serikali ya Zimbabwe ambao wanasoma ughaibuni kama njia mojawapo ya kuwaadhibu viongozi hao.
Adhabu hiyo imetolewa wakati
viongozi wa SADC huko Zamnbia wakiwa wakikubaliana kwamba hali ya Zimbabwe sio mbaya kama wamagharibi wanavyodai. Maamuzi ya Australia na yale ya viongozi wa SADC yanafuatana kama vile mabodia wanavyotupiana masumbwi moja baada ya jengine.
Wakati zoezi la kuwataja kwa majina, pamoja na anwani za wanapoishi watoto wa viongozi wa serikali ya Zimbabwe lilipozuka mwezi wa nne mwaka huu -
zoezi liliondaliwa na gazeti la Zimdaily msimamo wangu ulikuwa: sioni haki ya binaadamu mmoja kushinikizwa kwa kutumia binadamu mwingine. Kwamba ikiwa baba yangu ana makosa fulani basi na mimi nihukumiwe kwa makosa yale.
Nilitundika maoni pale kwa
Jikomboe, wengine walikuwa na mawazo tofauti. Nikichukulia mfano, kama mimi ningekuwa mmojawapo wa watoto wale, mwenye mawazo tofauti na baba yangu, pengine nimetumia skolashipu iliyoangalia uwezo wangu wa kimasomo, na ninafanya vizuri tu shuleni, halafu nizuiwe kuendelea na masomo kwa sababu baba yangu anafanya kazi serikalini… Haki yangu ya kuishi kama mtu huru itakuwa iko wapi.
Ninaelewa haki ya taifa lolote kuwa na uamuzi ni nani anayeweza kuishi katika mipaka yake nabaki na tatizo la kuelewa dhana ya haki za kibinadamu katika hili.