Wednesday, December 07, 2005

SIRI

Shhhhhh!.....tulia… Sikia nikupe siri ya siri. Naomba fanya hisani uitunze hii siri. Usiende ukisema kila mtu aifahamu siri. Na neno likienea mitaani nitajua nani aliosema na sitosita kukumaliza. Kwa siri.
1
Mipango ya kifo chako nitaifanya kwa siri. Watekelezaji wa kifo chako sitawaomba hisani kuificha siri kama nilivyokuomba wewe. Hao wataapa kiapo. Cha siri.
1
Wananijua. Na wanazijua nguvu zangu, na sheria nilizoweka kuificha siri. Hii siri yetu ya watu wawili. Kumradhi… siri ya watu mia.
1
Ndio najua. Lakini nimeamua hili jambo kulifanya siri. Kwamba siri zangu zinafananafanana na zenu kwa upande mmoja, vile zina asili ya aibu, ukatili, uongo, ujinga, makosa na dhalimu nyingine nyingine.
1
Lakini! lakini, lakini… mie siri zangu zina tofauti kubwa moja na zenu – siri zangu japo zinafanana na zenu mie nafanya yote haya ili kuleta mazuri. Sina nia mbaya asilani. Yote ninayofanya nayafanya ili kuleta mazuri kwetu sote. Na ndio maana nnataka muifiche hii siri.
1
Kwamba uhuru wa vyombo vya habari ni neno tu la kuwalaghai nyinyi mlioko mbali na jukwaa letu watawala. Huku kwetu uhuru wa vyombo vya habari hauruhusiwi kuvuka mipaka kutuingilia nguoni. Mimi pamoja na bunge letu la Uingereza tunayo sheria – Official Secrets Act - Na atakayevunja sheria hii , kama wale waliotoboa siri yetu mimi na bwana Bush ya kutaka kulipua kituo cha habari cha Al Jazeera, tutamkabili kisirisiri mpaka aache kazi ya kutangaza habari.
1
1
Na pale tulipoanzisha vita na mauaji ya hila kama huko Iraki, tutanunua vyombo vya habari kwa siri ili waongope na waendelee kutupigia propaganda ili kutufichia siri yetu.
1
Na wanahabari wakiendelea kutuelemea na utoboaji siri tutaanza kupayuka na kuwapakazia, mshirika wetu Rumsfeld ng’ambo ya Marekani keshaanza. Namtakia kila la heri.
1
Lakini kamwe hatutaungana mkono na serikali ya Tanzania kufungia gazeti la daima – kisa kumkejeli rais? Hatutaungana mkono na Serikali ya Tanzania kwa sababu serikali hiyo haifanyi dhalimu (kama tunavyofanya sisi huko nchi za umangani) ili kuendeleza demokrasia na kurekebisha hali za wananchi. Serikali ya Tanzania haiwatakii watu mema kama tunavyofanya sisi.
Fanya hisani. Tafadhali usiende mitaani kuwaeleza wengine hii siri – hakuna uhuru wa kweli wa vyombo vya habari.

5 comments:

Anonymous said...

Eee bwana we mwandani mwenyewe ni siri. na Naamini ni dhahabu ya Tanzania ambayo itaendelea kwa siri .Hasa kwa Watanzania utaendeleakuwa siri.Kama Mzee Zawose msanii ambaye Watanzania walitakiwa wajivunie anavyoendelea kuwa siri.Kama Ndesanjo Mtanzania ambaye ni bado siri.Kama Mti Mkubwa pale Helsinki anavyo endelea kuwa siri.Hivi imekuwaje Mzee Morisi nyunyusa kwa Watanzania bado siri?Simon

mloyi said...

Siri isifichuliwe au kupewa nguruwe wasiojua kula kimyakimya.
Siri huwa wanakaa nayo wenyewe, wakirisishana siri hiyohiyo, upo hapo?
Usishangae kuona ikulu wanarisishana kuna siri kubwa sana, ambayo wengine wakiijua wataleta balaa tupu.
Uchaguzi mwema.

Ndesanjo Macha said...

Ssssshhhhhhhhh...we! kimya...sauti ya chini...usimwambie yule...yule paleee, mwenye kofia nyeusi...hajui kuficha siri hata kidogo. Ukimwambia lazima amwambie mkewe, na mkewe lazima amwambie Zaina, yaani msusi wake, na Zaina anasuka wanawake sijui wangapi kwa siku na wote lazima awaambie...na ikifika kwa Mayasa basi dunia nzima imejua. Mayasa unajua ni shihata yule???

FOSEWERD Initiatives said...

halaaaleee na mie nimeijua lakini nitaistunza siri hakyanani walahi! hata mke wangu hataijua hiyo! nimwabie ili iweje? hivi mie ninajipenda kweli? na katoto kangu kagodo nitamudu kukakuza kweli?? sawa hata kama janjaweed walifanyiza? we inakuhusu nini? kwani we ulaji wako hupati/ ona kwani wakorofi si wanaula wa chuya? si unaona huyo mmgine alimuua mwana hizbu amehakikishiwa pepo? we si unaona gharama za afya zilivyopanda? na za elimu pia ukisema sema utayamudu kweli? ibakie siri tena top secret!

lnwslot789 said...

ดูหนังออนไลน์ กับหนังออนไลน์ที่คมชัดเต็มระบบงทั้ง 4K HD สนุกง่ายๆ กับ The Beast ปิดโซลล่า (2019) [ พากย์ไทย ]