Saturday, March 10, 2007

WOMADELAIDE 2007

(wazawa wa Adelaide - Kaurna - wakibariki tamasha)
1

Wikiendi hii tumerejea tena kwenye moja ya matamasha maarufu ya muziki wa kimadunia katika Australia - Womadelaide 2007. Mwaka huu tamasha hili ni la 15 hapa Adelaide na kwa mara ya kwanza kumekuwa na ratiba tofauti. Katika siku tatu za tamasha hili wanamuziki wote vinara wanatumbuiza mara moja tu. Haidhuru.
1
Bila kujali joto la kiangazi wapenzi wasiopungua 70 elfu wameshaanza kuburudika ndani ya viwanja vya Adelaide botanic park na wataburudika kwa siku tatu mfululizo mpaka nyasi kugeuka vumbi.
1
Pamoja na wanamuziki wa Kiafarika kama Femi Kuti (Nigeria), Salif Keita (Mali) na Mahotella Queens (Afrika ya Kusini) magwiji wengine kutoka pande zote za dunia kama akina Asha Bhosle (India); Kronos Quartet (US); Blue King Brown (Australia); Gotan Project (France / Argentina); Lior (Australia); Lunasa (Ireland); Emma Donovan Band (Australia); na Mariza (Portugal) watatumbuiza pia.
1
Kwa upande wangu mpaka hivi sasa nimeshahudhuria maonyesho ya bendi mbili za kutoka Afrika: Mahotella Queens na Femi Kuti and the Positive Force. Na bila ubishi wowote Mahotella Queens wamenisuuza moyo vilivyo.

(Bi mkubwa wa ki-Kaurna akisoma risala ya kubariki tamasha na kuwaenzi wenye nchi)
1
Kama ilivyo mila na desturi ya hapa Australia haianzi shughuli bila kutoa heshima kwa wazawa wa nchi hii wanaotambulika kama Ma-aborijino au Indigenous people ambao walikuwa 'hawatambuliki' kama binaadamu kamili kabla ya mwaka 1967.
1
Wazawa walianza kwa kutoa heshima ya ki-kaurna (inatamkwa ga-na). Mzee wa kabila (kama anavyoonekana pichani) alianza kusoma dua za kikwao akafuatiwa na vijana waliocheza ngoma ya kubariki tamasha. (juu kabisa pichani)

MAHOTELLA QUEENS (Womadelaide 2007)

(Mahotella Queens - Womadelaide 2007)
1
Mahotella Queens ndio waliofungua dimba ya tumbuizo kwenye tamasha la 15 la Womadelaide. Baada tu ya baraka za ufunguzi, bila kuchelewa kikosi cha maajuza watatu kutoka Afrika ya kusini, Mahotella Queens walivamia jukwaa namba moja na kuporomosha vibao vyao vyote maarufu - pamoja na Kazet na Umuntu Ngumuntu. ilikuwa onyesho kabambe - kwa lugha ya wanamiziki wanasema walipiga "tight set".
12
Miye naona hii ni baraka kuwashuhudia maajuza hawa wakitumbuiza, kwani walisharitaya shughuli za muziki baada ya kupotelewa na wanamuziki wenzao watatu wakiwemo Mzee Mahlatini na West Nkosi. Naona ni baraka vile hawa madada wazee - Hilda Tloubatla, Nobesuthu Shawe Mbadu na Mildred Mangxola ndio historia ya muziki wa dansi wa Afrika ya kusini. Hawa ndio hasa waliokuwamo kwenye kuipika mbaqanga jive.
1
Na kama alivyokuwa akieleza Bibie Hilda Tloubatla akiwa jukwaani - bila kujituma, kukaza nia tena baada ya kukata tamaa na misiba pengine wasingelikuwapo ndani ya tamasha mwaka huu.

Shoo yao ilikuwa swafi sana - walikuwa na mpigaji gitaa zito, mpiga gitaa, mpiga ngoma (yaani "drums") na mpiga kinanda tu. Hata hivyo vibibi hivi vilitoa vichekesho na mawaidha kwa wanawake na wanaume.
1
Usia ambao pengine haukuwafikia vizuri watoto wadogo na vichwa maji wengine ni pale walipowaambia akina mama: "Mkitaka kuwa na afya na furaha, muweze kucheza kama sisi mpaka uzeeni, siri ni kujidamka alfajiri ya saa kumi, umpe mumeo staftahi, na akirejea kutoka kazini akute maakuli, basi mumeo mwenyewe atakuwa akiwahi kurudi nyumbani kila siku, na kama ana uwezo atakununulia chochote unachotaka". Ma-feminist walinung'unika na kauli.

FEMI KUTI AND THE POSITIVE FORCE (Womadelaide 2007)

(Femi Kuti akitumbuiza Ijumaa usiku 9-3-07)

Shoo nyingine ya kutoka Afrika hapa katika Tamasha ni ile ya mwanamuziki Femi Kuti wa Nigeria. Bila ya shaka hii ilikuwa ndiyo bendi kubwa kupita zote usiku wa Ijumaa. Kulikwa kuna waimbaji, wapiga midomo ya bata ya aina zote (trumpets, alto na tenor sax, trombone, nk.) wapiga ngoma wawili, wanenguaji watatu, wapiga magitaa wawili, na mpiga gitaa zito, mpiga vinanda… pamoja na Femi mwenyewe ambaye anapuliza midomo ya bata ya aina mbili pamoja na kupiga kinanda na kuimba, kuunguruma na kufoka.
1
Onyesho lake lilikuwa ni nguvu na sauti kubwa mno. Ilikuwa kama vile amefunga vipaza sauti vya shoo za rock 'n' roll au heavy metal. Niliwaona wazee wachache wakihama mistari ya mbele huku wakiziba masikio.

Shoo ya femi ilikuwa sawa na kumsikiliza baba yake - Fela. Kulikwa na mseto wa Afro-beat na jazz ya haraka haraka. Alitoa maneno makali dhidi ya Obasanjo na viongozi wengine wa Kiafrika. Kadhalika aliwasuta waafrika waliokuwapo uwanjani, na kuwahimiza kufanya kweli. Ukiopndoa kibao cha Do Your Best na Beng Beng Beng, vibao vyote vilikuwa ni vya kisiasa.
1
Huyu bwana Femi alitoa sare na ma-Aborigine katika kupuliza sax. Ma-aborigines wanajulikana kwa mtindo wao wa kupiga digderidoo (aina ya filimbi kubwa yenye sauti nzito) huku wakitumia circular breathing. Femi alionyesha umahiri huo kwa kupuliza mlio mmoja wa sax kwa dakika kama mbili na nusu bila kukata.

Pamoja na kupenda sana kuangalia wanenguaji wa kike, mtindo wa wananguaji wa Femi wa kuwapa mgongo watazamaji huku kitambaa (au kijichupi) kikiwa kinavuka na kuonyesha msamba mara kwa mara kidogo kilinifanya nifadhaike. Vinginevyo ile dansi yao maarufu kana kwamba wanafanya mapenzi na mwanamume nadhani iliwavutia wengi pamoja na wapiga picha waliojazana upande wa wanenguaji.

Baada ya onyesho nilimkuta Msenegali mmoja anayepiga muziki hapa Adelaide, Lamin, akibishana na wazungu juu ya Femi. Wazungu wanadai waliupenda sana ule muziki kwani 'the whole stage was busy, the man's got energy, oooh!" Msenegali alikuwa anadai kuwa hakuweza kuucheza mziki ule kwa filingi.