Monday, May 07, 2007

CHEMA HAKIDUMU

Chema hakidumu kingekupendeza
Ungawa na hamu kukingojeleza
Saa ikitimu kitakuteleza


Chema wangu babu Kibwana Bashee
Alojipa tabu kwamba anilee
Illahi Wahabu mara amtwee


Hizo beti mbili nilizikariri zamani kutoka kwenye kitabu cha Abdilatif Abdala "Sauti ya Dhiki". Na kama ninavyozikumbuka zimekuwa zinanizinga mawazoni kwa masiku kadhaa sasa.

Nimeingiwa na machungu na woga. Uwezo wangu wa kufikiri au kutatua matatizo yaliyonifika umeniponyoka. Maisha yamenikumbusha uwanaadamu wangu. Kinachonisukuma ni ule moyo wa stahamali tu. Na ninaomba nijaaliwe stahamali zaidi.

Kitambo kidogo kilichopita Mwenyezi Mungu alimtwaa kipenzi Mama yangu Mkubwa, Kadala. Marehemu Kadala nilikuwa naye karibu sana wakati wa utoto wangu.

Naam, ndio maisha. Na hapa nilipo maisha mengine yanaenda kwa kasi ya mwendo wa radi. Nakimbiakimbia, ninachakurachakura kama kuku kutwa nzima. Kukicha naanza tena kama jana. Ndio maisha.

Basi naona bora kukawia kuliko kuiwacha safari. Tupo wote safarini japo tunaonana kwa nadra bloguni. Mambo yakisawazika bila ya shaka nitaongeza kasi na huku kwenye mitandao pia.

Haidhuru. Kule kwenye kurasa za Global Voices baada ya muda kama mwezi hivi kuna muhtasari wa blogu za kiswahili uliopandishwa leo. Tafadhali tupa jicho na huko pia. Bila kusahau kuperuzi kidogo kwenye ukurasa wa Reuters Tanzania.

7 comments:

Simon Kitururu said...

Mzee!Tukopamoja!Endeleza tu uendelezayo.Ingawa tunakumisi lakini tunaelewa.Mimi binafsi kuchelewa kwako kubandika, kumenipa muda wakurudia makala zako nyingi baabu kubwa ulizoziandika zamani mara nipitapo hapa .

Hector Mongi said...

Pole sana Joe. Nami niliposoma shairi lako nilikumbuka mistari michache niliyosoma nikiwa darasa la sita au la saba hivi. Mwandishi simkumbuki ila nakumbuka alikuwa akiwalilia wahenga katika fani ya utunzi:

Waandishi mashughuri, pamoja na wanazuo,
Hodari wa kufikiri, kutunga yenye mafao,
Ilipofika safari, kwenda kusiko rejeo,
Hawakuwa na saburi, wote wamekwenda zao.


Walikuwa wapendezi, wakifadhili wenzao,
Wakapendwa kwa mapenzi, ajabu mfano wao,
Wote hao wamezama…, zimebaki sifa zao,
Kwa kilio na machozi, hawarudi watu hao.


Naam. Hatuna la kufanya pale aliyetoa anapoamua kutwaa kilicho chake.
Ndio njia yetu sote. Poleni sana.

Anonymous said...

Mwandani,
Pole sana.Kama ulivyonena,ndio maisha.Endelea kuipigania nafsi kwa sababu kama wasemavyo wale weusi wenzetu a mind is a terrible thing to waste!Tupo pamoja.

Mija Shija Sayi said...

Poleni sana Mwandani, MtiMkubwa na familia kwa ujumla.

Mija Shija Sayi said...

Nambiza pitia mjadalani uchukue fomu.

Anonymous said...

Pole Sana

mwandani said...

Nawashukuruni nyote kwa kunitakia pole.

Mija nashukuru kwa mwaliko wako.

Ikesha umenifurahisha sana na shughuli yako ya uhamasishaji umma vile umegonga milango mingi na kushawishi wanablogu wagombee nafasi. Hivyo ndivyo kuwafikia wananchi - nadhani matokeo yake umeyaona.
NB: Si ungejipendekeza katika nafasi ya katibu mwenezi - lakini uweka hazina nao sawa...(masihara!)